HABARI

AZAM FC:MSIMU HUU USHINDANI NI MKUBWA

 


 KOCHA msaidizi wa Azam FC amesema kuwa ushindani ndani ya Ligi Kuu Bara ni mkubwa kwa kuwa kila timu inapambana kufikia malengo iliyojiwekea.

Msimu wa 2020/21 Azam FC ilianza kwa kasi na ilicheza mechi 7 mfululizo bila kuonja ladha ya kichapo huku ikiwa inaongoza ligi kabla ya kutunguliwa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, Uwanja wa Jamhuri.

Kwa sasa kinara ni Yanga ambaye amecheza mechi 21 na amekusanya pointi 49 kibindoni anafuatiwa na Simba nafasi ya pili na pointi zake ni 42 na imecheza mechi 18.

Vivier Bahati ambaye anafanya kazi kwenye viunga vya Azam Complex akiwa msaidizi wa George Lwandamina ambaye ni Kocha Mkuu wa timu hiyo amesema kuwa bado wanaendelea kupambana.

Timu hiyo kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ipo nafasi ya tatu ikiwa imecheza jumla ya mechi 21 na imekusanya pointi 37.


Imetupia jumla ya mabao 29 na kinara wa utupiaji ni Prince Dube mwenye mabao 7 na pasi tano za mabao kwenye akaunti yake.

Mchezo wake uliopita ililazimisha sare ya bila kufungana na timu ya Tanzania Prisons iliyo nafasi ya 8 na pointi 26 baada ya kucheza jumla ya mechi 20. Ulichezwa Uwanja wa Azam Complex.

Bahati amesema:”Ushindani ni mkubwa na kila timu inapambana kufikia malengo yake hicho ndicho ambacho nasi pia tunakifanya ndani ya uwanja.

“Wengi wanapenda kuona matokeo mazuri kutoka kwetu hilo lipo na linawezekana hivyo mashabiki waendelee kutupa sapoti kwani kila kitu kinawezekana,”.

About the author

kidevu

Leave a Comment