HABARI

“Nchi iko salama Watanzania wachukue tahadhari” Serikali

Serikali imesema tayari imechukua hatua kadhaa za tahadhari ili kukabiliana na maambukizi ya Virusi vya Corona na kwamba kwa sasa nchi iko salama.
Kauli hiyo ya serikali imetolewa jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt Hassan Abbasi wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari.
Amesema kuwa serikali inaendelea kufanya jitihada mbalimbali kuhakikisha virusi hivyo vya corona sio tu haviingii nchini, lakini pia kuzuia kusambaa kwa maambukizi endapo vitaingia.
“Zipo hatua zinazochukuliwa ndani ya taasisi na wizara moja moja, lakini pia zipo hatua za kitaifa za kukabiliana na virusi hivyo, na hivyo naomba kuwatoa hofu Watanzania kuhusu corona” Dkt. Abbasi.
Ametaja miongoni mwa hatua hizo kuwa ni ile ya serikali kuandaa utaratibu maalumu katika maeneo ya viwanja vya ndege na maeneo ya mipakani, ambapo watu hawapimwi homa ya corona bali joto la mwili ili kuangalia endapo joto limezidi kiwango cha kawaida cha binadamu.
“Watanzania waendelee kuchukua tahadhari kama Rais John Magufuli alivyoeleza na wazingatie maelekezo ya namna ya kujikinga yanayoendelea kutolewa na Wizara ya Afya kupitia wataalamu wake” Msemaji huyo wa Serikali.
Amesema hatua nyingine iliyochukuliwa na serikali kuhakikisha inakabiliana na maambukizi ya virusi vya corona ni kuandaa vituo maalumu vya kuwatenga washukiwa, vituo ambavyo vina vifaa vyote vya kupima ugonjwa huo.
Dkt Abbasi ametumia mkutano wake na waandishi wa habari, kuvipongeza vyombo vya habari nchini kwa kuitikia wito wa Rais Magufuli wa kuhabarisha umma kuhusu virusi vya corona.

About the author

kidevu

Leave a Comment