HABARI

TBS yasisitiza usajili wa majengo ya chakula na vipodozi

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limemaliza Kampeni yake ya kutoa elimu kwa umma katika Wilaya za Mpanda, Rungwe na Ludewa kuhusiana na usajili wa majengo ya chakula na vipodozi, umuhimu wa kusoma taarifa zilizopo kwenye vifungashio vya bidhaa ikiwamo muda wa mwisho wa matumizi wa bidhaa.
Kupitia kampeni hiyo maofisa wa shirika hilo walielimisha jamii kuhusu umuhimu wa kununua bidhaa zilizothibitishwa ubora na TBS.
Kampeni hiyo ya elimu kwa umma imefanyika katika wilaya hizo kuanzia mwanzoni mwa wiki iliyopita ikihusisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na wananchi kwa ujumla.
Pia kampeni hiyo iliendeshwa kwenye masoko, stendi, minadani na maeneo mengine ya wazi ambapo wananchi walijitokeza kwa wingi kupata elimu hiyo pamoja na ufahamu wa masuala mbalimbali yahusuyo ubora wa bidhaa.
Akizungumza wakati wa kampeni hiyo Mkaguzi wa TBS,Ernest Simon, aliwahimiza wananchi kujenga utamaduni wa kununua bidhaa zilizothibitishwa ubora wake na TBS ili kuepuka hasara kwa kupoteza fedha kununua bidhaa ambazo hazina ubora na kuwa hatarini kupata athari za kiafya.
Aliwakumbusha wananchi kwamba vita ya bidhaa hafifu sio ya TBS pekee, bali ni ya Taifa kwa ujumla.
“Kampeni hii imeweza kuwafikia walengwa zaidi ya 8,000 kati yao wajasiriamali wakiwa ni 64, wanafunzi wa shule za msingi na sekondari 4,381 na wananchi 3,658,” alisema Simon.
Aliwasisitizia wafanyabiashara kuhusiana na umuhimu wa kusajili majengo yao kupitia mfumo unaopatikana kwenye tovuti ya shirika hilo na wananchi waendelee kutoa taarifa kupitia mawasiliano waliyopewa pale wanapogundua uwepo wa bidhaa hafifu katika soko.
Wakati wa kampeni hiyo maofisa wa shirika hilo walipata fursa ya kuhamasisha wajasiriamali wanaojihusisha na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo za nafaka, sabuni,mikate, maziwa, pilipili,siagi ya karanga,mvinyo,mafuta ya kula,asali na unga lishe kuhusu utaratibu wa kupata leseni ya kutumia alama ya ubora ya TBS bure.
Kampeni hiyo ni endelevu na itaendelea katika Wilaya za Rombo Lushoto na Hanang
 
 

About the author

kidevu

Leave a Comment