Jaji Mkuu nchini humo David Maraga amesema kuwa mahakama inasitisha uendeshaji wa kesi ndogondogo mwa muda wa siku 14
Sekta ya mahakama nchini Kenya imechukua hatua ya kufunga baadhi ya shughuli zake kufuatia taarifa ya kupatikana kwa mtu wa kwanza mwenye virusi vya corona nchini humo.
Akizungumza na waandishi wa habari Jaji Mkuu nchini humo David Maraga amesema kuwa mahakama inasitisha uendeshaji wa kesi ndogondogo mwa muda wa siku 14.
Aidha amesema kuwa wafungwa waliopo rumande hawatafikishwa mahakamani na badala yake wenye makosa madogo madogo watatozwa faini katika kituo cha polisi, kulingana na mwongozo utakaotolewa na Kamishna Mkuu wa polisi.
Amesema kuwa majaji hawatapewa mafunzo kwa kipindi cha siku 14 na safari za nje ya nchi zimesitishwa.
Wakati huo huo makazi ambako aliishi mtu aliyepatikana na Coronavirus yamekuwa yakinyunyiziwa dawa ya kuua wadudu na wale waliobainika kuwa wametangamana na mgonjwa huyo wametengwa kwa ajili ya uchunguzi.
Hali ya wasi wasi imetanda nchini humo kufuatia kutangazwa kwa kisa cha kwanza cha mlipuko wa coronavirus, huku baadhi ya wakazi wa jiji la Nairobi wakionekana kununua bidhaa kwa wingi kwa hofu ya kuzikosa baadae iwapo mlipuko utaendelea kusambaa.
Upande wa kesi kubwa mahakama imesema kuwa zitahudhuriwa na wahusika wa kesi pamoja na mawakili wao, na usalimianaji wa mikono na kukumbatiana vimepigwa marufuku katika maeneo ya mahakama.
Siku ya Ijumaa waziri wa afya nchini humo Mutahi Kagwe alitangaza kwamba mtu mwenye maambukizi ya virusi vya Corona alithibitishwa Alhamisi usiku.
Kisa hicho ni cha raia wa Kenya aliyewasili nchini humo kutoka Marekani kupitia mjini London nchini Uingereza tarehe 5 mwezi Machi 2020.
Aligunduliwa kuwa na virusi hivyo katika maabara ya wizara ya afya nchini Kenya.
Hatahivyo waziri huyo wa afya alisema kwamba mgonjwa huyo ambaye ni mwanamke yuko katika hali njema na kwamba viwango vyake vya joto vimeshuka na kuwa vya kawaida.
Aliwahakikishia Wakenya kwamba Kenya imejiandaa vilivyo kukabiliana na virusi hivyo tangu kisa cha kwanza kitangazwe nchini China, akiongezea kuwa serikali itatumia raslimali zake zote kukabiliana na janga hilo.