Kaimu Mkurugenzi Mkuu TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Mbungo, amewasimamisha kazi watumishi wawili wa Taasisi hiyo akiwemo Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga Christopher Mariba kwa tuhuma za rushwa.
Aliyekuwa Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga Christopher Mariba
Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, Jenerali Mbungo amesema Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga Christopher Mariba na Hilton Njau ambaye ni Afisa Uchunguzi mkuu kutoka Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Tanga wonadaiwa kuomba rushwa.
‘Hilton Njau anatuhumiwa na kosa la kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa mmoja wa watuhumiwa waliokuwa wakichunguzwa na TAKUKURU, jambo ambalo ni kinyume na kifungu cha 15 cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na rushwa Na. 11 ya mwaka 2017’, imeeleza taarifa hiyo.
Aidha Kaimu Mkurugenzi Mkuu TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Mbungo, amemteua Dkt Sharifa Bungala kukaimu nafasi ya Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga, baada ya Christopher Mariba ambaye alikuwa akishikilia nafasi hiyo kusimamishwa kwa tuhuma za rushwa.
Ameongeza kuwa baada ya uchunguzi kukamilika watuhumiwa hao watakuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, huku wakiwoanya watumishi wengine wa taasisi hiyo kuwa waadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao.