HABARI

BERNARD MORRISON AENDE YANGA KWA MKOPO

 WAKATI mwingine unaweza kupata kila kitu kwenye maisha yako ila ukakosa matumaini hapo matatizo yanaanza hasa kwa mmiliki wa kile ambacho anacho na yule ambaye anahitaji kumiliki.

Hasa pale mitaa ya Kariakoo kumekuwa na mambo ambayo yanatokea na ukisikiliza kila mmoja anavutia kamba upande wake ili kuonekana yupo sawa na kusahau kwamba mpira ni dakika 90.

Unamkumbuka yule mwamuzi ambaye alichezesha mchezo wa Tanzania Prisons 1-0 Simba, alifungiwa na Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) kwa kosa la kushindwa kuumudu mchezo ule.

Mchezaji ambaye analeta mgogoro kwenye ligi, Bernard Morrison ambaye yupo zake Simba kwa sasa alionekana akichezewa faulo ndani ya 18, mwamuzi akapeta na maisha yakaendelea kama kawaida.

Unamkumbuka yule mwamuzi wa KMC 1-2 Yanga, ile penalti matata iliyotolewa kwa Yanga baada ya Michael Sarpong kuangushwa ndani ya 18 maisha yake yapoje na namna gani alilamikiwa na wapinzani.

Weka kando kwamba kuna mechi ya Mbeya City 1-1 Yanga, bao lilionekana na utata na kuna penalti ya Yanga ilipaswa kutolewa ila ikapetwa na Mbeya City walipata penalti wakafunga.

Bado maisha yanaendelea rudi nyuma pale Gwambina Complex, Gwambina 0-0 Yanga, Gwambina walifunga bao likafutwa kwa kile kilichoelezwa kuwa kuna mchezaji wa Gwambina alikuwa ameotea.

Kabla ya bao hilo kufungwa inaonekana dhahiri kona waliyopata Gwambina ilikuwa na utata mwisho wa siku bao lake nalo likaleta utata.

Haya maisha ya Kariakoo ni magumu kwa kweli sijajua tatizo lipo wapi. Labda ningependa kuwashauri Simba wamrudishe Morrison kwa Yanga iwe kwa mkopo ama kwa kupenda ili kupunguza hizi filamu za kila siku.

Ndio labda tatizo ni Morrison kwa sababu kila atakavoboronga ama kufanya vizuri utaskia watu wanazungumza na kuanza kutoa yale ya moyoni.

Huyu Morrison ni tatizo kubwa kwenye soka letu na sio kitu kingine mimi ninadhani ipo hivyo ama wewe unadhani kuna tatizo gani. Nadhani unakumbuka kuna mchezo pale Uwanja wa Mkapa alitoa pasi kwa mgongo unajua siku ya pili nini kilitokea, sijui nikumbushe.

Ila kwa nini Simba hawaonekani kulalamika kuhusu waamuzi wao wanaendelea na maisha yao kama kawaida ndani ya uwanja na nje ya uwanja wanajua wao.

Hapo kuna kitu cha kujifunza na kuona namna gani maisha yanaweza kuendelea bila uwepo wa malalamiko katika kutafuta haki.

Yanga waliweka wazi kwamba huenda wangejitoa kushiriki ligi ikiwa mwamuzi wa mchezo wa Februari 20 kati yao dhidi ya Yanga asingetenda haki. Huku ni mbali sana tunafika.

Bado sijui haya mawazo yapoje labda tusubiri na tuone ila mchezo ndani ya uwanja unahitaji maandalizi na kila mmoja ni lazima atambue kwamba mwamuzi naye ni binadamu makosa yapo hata Ulaya ndio maana wanatumia VAR ila simaanishi wasifanye vizuri.

Bado soka letu ni pasua kichwa, waamuzi pasua kichwa ,viongozi wengine pia ni pasua kichwa kuna kazi kubwa kuyafikia mafanikio.

Makala haya iliandikwa ndani ya Gazeti la Championi na Oscar Oscar.

About the author

kidevu

Leave a Comment