Ujerumani imerikodi takriban visa vipya 15,030 vya maambukizi ya virusi vya corona huku idadi ya vifo hadi jana ikifikia 44.
Taarifa hizo zinazojumuisha majimbo yote 16, zinaonyesha kwamba jimbo lenye idadi kubwa ya watu la North-Rhine Westphalia limeripoti zaidi ya visa 4,970, likifuatiwa na Bavaria lenye visa 2,280 na Baden-Wuerttemberg lenye zaidi ya visa 2,740.
Kutokana na hali hiyo askari wa akiba ambao wako nje ya jeshi wameanza kuripoti kazini kwa hiari huku Waziri wa Ulinzi Annegret Kramp-Karrenbauer akisema jeshi linajiandaa kupambana na mgogoro wa virusi vya corona.
Lakini waziri huyo pia ameonya dhidi ya matarajio makubwa akisema jeshi na hospitali zake zilizo na madaktari wapatao 3,000 ni sehemu ndogo tu ya mfumo wa afya wa Ujerumani.