Baada ya serikali mkoani Njombe kutoa maelekezo na kupiga marufuku matukio ya sherehe za harusi na misiba kuhusisha watu wengi ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya CORONA (COVID-19),viongozi wa madhehebu mbalimbali na wenyeviti wa serikali za mitaa na vijiji mkoani humo wamekiri na kuja na utaratibu mpya utakaokuwa ukitumika ili kuepukana na maambukizi hayo.
Wakiweka bayana hatua walizochukuliwa katika uendeshaji wa ibada za harusi na misiba viongozi wa dini akiwemo mchungaji Gabriel Nduye makamu askofu wa K.K.K.T dayosisi ya kusini na Zephania Tweve mchungaji kiongozi wa kanisa la T.A.G mkoa wa Njombe wanasema wamepunguza muda wa ibada zoezi ambalo limekwenda sambamba na kusitisha utaratibu wa kupeana mikono wakati wa kuagana.
Kuhusu Ibada za harusi na misiba viongozi hao wa dini wanasema walishatangaza kwa waumini katika matukio hayo kuhusisha watu wachache wa muhimu wakiwemo ndugu na kisha sherehe kwa matukio ya harusi kupangwa baadae huku kwa mikasa yaa misiba jamaa na marafiki wakitakiwa kwenda kutoa pole mara baada ya maziko na wengine kusitisha kabisa.
“Tumetoa maelekezo na kuyasimamia harusi zifanyike kwa maana ya ibada lakini sherehe zifaate maelekezo ya serikali kwamba hakuna mikusanyiko inayohitajika isiyo yalazima,kwenye matukio ya vifo bado nako tumeweka utaraibu pia hakutakuwa na mikusanyiko ya watu”alisema Gabriel Nduye na Zephania Tweve
Kwa kuwa katazo hilo limewataka wenyeviti wa mitaa ,vijiji na vitongoji kutumia nafasi zao kuelimisha watu wanaowaongoza ikiwemo kuachana na utamaduni wa kushiriki kwa wingi katika matukio ya misiba.Mwenyekiti wa mtaa wa Mpechi Onesmo Kilasi anaeleza jinsi lilivyopokelewa na kutoa msimamo wa mtaa wake juu ya mapambano dhini ya mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19.
“Sio rahisi kwamba mtu akifiwa basi ndugu wa karibu na majirani asifike kwenye msiba,isipokuwa sisi viongozi tutajitahidi tueleze kinaga ubaga kwamba kutokana na hali ilivyo ya maradhi angalau tupungeze mikusanyiko,hilo lazima tufanye”alisema Onesmo Kilasi
Lakini kwa upande wa baadhi ya wananchi mjini Njombe akiwemo Geofrey Kaduma na Kamilo Ilomo wanasema licha ya kuwa ni ngumu kubadili utamaduni wa watu uliyozoeleka ni lazima kwasasa kukubali na kuendana na mazingira tuliyonayo.
“Mila na tamaduni zetu tulizozioea inaweza ikawa ni ngumu hata kuyakubali haya ya kuepuka mikusanyiko na mengine,lakini kutokana na janga tulilo nalo inabidi tutembee katika nafasi ya kujiokoa” alisema Geofrey Kaduma
Hadi sasa idadi ya wagonjwa wa CORONA imefikia 13 kwa mujibu wa taarifa ya serikali iliyotolewa na waziri wa afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto Ummy Mwalimu na wote wakiendelea vizuri huku mgonjwa wa kwanza aliyegundulika na maambukizi ya COVID-19 akiwa amepona.