Rais wa Marekani, Donald Trump amefanyiwa vipimo vya Virusi vya Corona na kugundulika kuwa hajaambukizwa ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa daktari wa Ikulu ya Marekani, Sean P. Conley amethibitisha taarifa hizo, na kusema rais Trump aliamua kufanyiwa vipimo siku ya Ijumaa baada ya kukaribiana na afisa wa Brazil ambaye aliambukizwa COVID-19.
Rais Trump ametangaza kuziongeza Uingereza na Ireland katika orodha ya nchi ambazo abiria wake wamezuiliwa kuingia Marekani.
Hapo awali marufuku hiyo iliwahusu abiria wa mataifa ya Ulaya. Huko Uhispania serikali inapanga kuwafungia raia wake karibu milioni 46 kuanzia kesho Jumatatu kama sehemu ya mpango wa hali ya dharura wa siku 15 kukabiliana na mripuko.
Ufaransa imeyafunga maduka, migahawa na maeneo ya burudani kuanzia leo Jumapili huku raia wakielezwa kubakia nyumbani huku kesi za maambukizi zikiongezeka mara mbili katika muda wa saa 72.