Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres jana alipokea taarifa nzuri kutoka kwa vyama vya Libya vinavyozozana. Taarifa hiyo inahusu kusimamisha kwa muda mapigano ili nchi hiyo iweze kupambana na changamoto ya janga la maambukizi ya virusi vya corona.

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, hofu ya virusi hivyo vipya vya corona imeenea nchini Libya. Serikali imewaamrisha watu wote kubakia majumbani wakati wote tangu jana usiku.
Vikosi vya kamanda muasi wa kijeshi Khalifa Haftar anaedhibiti upande wa mashariki mwa nchi hiyo, vina wasiwasi kwamba wanajeshi wa kigeni wanaowasaidia kupigana vita hivyo huenda wakawa wameambukizwa virusi hivyo.
Libya imetumbukia katika machafuko na kugawanyika katika makundi tangu mwaka 2011, kulipozuka vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivymuondoa kiongozi wa muda mrefu Moammar Gadhafi, aliyeuawa baadaye.