HABARI

Mahakama yafafanua faini na Rais Magufuli kwa Mbunge wa Chadema Peter Msigwa

Baada ya Rais John Magufuli kumlipia faini ya Sh38 milioni, mbunge wa Iringa Mjini, mchungaji Peter Msigwa, Chadema waliomba fedha zilizolipwa benki kwa ajili ya mbunge huyo zitumike kumlipia faini mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.

Msigwa na viongozi wengine wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe, waliamriwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kulipa faini baada ya kuwatia hatiani kwa makosa ya kufanya mkusanyiko na maandamano yasiyo halali na uchochezi.
Juzi Rais Magufuli alimlipia Msigwa faini ya Sh38 milioni kati ya Sh40 milioni alizotakiwa kulipa mbunge huyo ili atoke jela baada ya familia yake kuchangishana Sh2 milioni. Hata hivyo, malipo kwa mchungaji Msigwa, yaliibua mjadala baada ya kutolewa taarifa mbili tofauti kuhusu kumlipia faini .
Taarifa hizo mbili ziliibua utata, huku watu wakihoji ilikuwaje mbunge huyo akalipiwa faini mbili tofauti, wakati namba ya malipo ya pesa hizo (control number) kutoka mahakamani kwa kawaida huwa ni moja tu kwa kila mtu anayetaka kufanya malipo.
Jana, Mahakama ya Kisutu ilitoa ufafanuzi wa mkanganyiko huo, ikibainisha kuwa malipo yaliyoanza kuwasilishwa mahakamani hapo ni ya Rais Magufuli.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Godfrey Isaya aliliambia Mwananchi kuwa namba ya malipo ya faini ya mtu aliyehukumiwa kulipa faini, huweza kutolewa kwa watu zaidi ya mmoja na kwamba hilo si tatizo.
Alisema namba ya malipo, inakubali malipo kama kawaida na huingia katika mfumo ambao unaweza kutambulika na hata kama mtu akifanya kosa lingine akahukumiwa, akilipa faini atapewa ‘control namba’ hiyo hiyo kulipia.
Alifafanua kuwa malipo hayo huingizwa kwenye mfumo wa kumbukumbu za mahakama baada ya mlipaji kuwasilisha risiti ya benki ya malipo husika.
“Kwa hiyo malipo yaliyoingia kwanza kwenye`system’ ni ya Rais Magufuli na sisi hayo ndiyo tuliyoyapokea na kuyaidhinisha,” alisema Hakimu Isaya.
Alisema kutokana na hali hiyo, uongozi wa Chadema uliwasilisha maombi mahakamani hapo ili malipo waliyolipa kwa Mchungaji Msigwa yahamishiwe kwa Heche. Alisema kuwa maombi hayo ya kubadilisha malipo yaliwasilishwa mahakamani hapo na mwanachama wa Chadema, Evans Luvinga kwa niaba ya chama hicho na kwamba yeye aliona maombi hayo jana.
“Hivyo na sisi kama mahakama tumekubaliana na maombi hayo na taratibu hizo zimeshafanyika,” alisema Hakimu Isaya.
Ofisa habari wa Chadema, Tumaini Makene akizungumza na Mwananchi jana alikiri chama hicho kuwasilisha ombi la kuhamishwa kwa fedha hizo.
Kuhusu nani aliyetangulia kufanya malipo, Makene alisema Chadema walichukua namba za malipo siku ya pili baada ya hukumu na kufanya malipo mapema juzi.

About the author

kidevu

Leave a Comment