HABARI

China yatoa kauli kuhusu nguo za wagonjwa wa Corona

Ubalozi wa China nchini Tanzania umekanusha taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba, nguo za watu walioathirika na Virusi vya Corona nchini China, zinasafirishwa na kuletwa Afrika, hivyo watu wazipuuze kwani zinataka kuleta mgawanyiko kati ya China na Afrika.
Taarifa hizo zimetolewa kupitia ukurasa wa Twitter wa Ubalozi huo nchini na kueleza kushangazwa na uvumi huo na kwamba Taifa hilo limekuwa likiwatunza vizuri raia wa Afrika wanaosoma nchini humo, tangu mlipuko wa ugonjwa huo uanze mwishoni mwa mwaka 2019.
“Inajulikana kabisa sio Taifa la China tu bali kuna Mataifa mengine ambayo nguo hutoka huko na kuletwa Afrika, wafanyabiashara wengi wa Kiafrika wanatueleza inavyowawia vigumu kuagiza bidhaa kutoka China, kwahiyo inawezekanaje nguo za waathirika wa COVID-19 kuja Afrika kwa sasa?” imeeleza taarifa hiyo.
Kumekuwepo na taarifa mbalimbali katika mitandao ya kijamii, zikitoa tahadhari ya kuacha kununua nguo zinazotoka China kwa kipindi hiki kwa kuwa nyingi zilizopo kwa sasa ni za waathirika wa Virusi vya Corona.

About the author

kidevu

Leave a Comment