Mke wa Riek Machar anasema mume wake hawezi kufanya ziara za ndani ya nchi kwa uhuru
Mke wa makamu wa rais wa Sudan Kusini aliyeapishwa hivi karibuni Riek Machar anasema mume wake anahisi “ni kama mfungwa”.
Angelina Teny, ambaye binafsi ni waziri wa zamani katika serikali ya Sudan Kusini, ameiambia BBC kwamba masharti yaliyowekwa na Mamlaka ya kimaendeleo ya serikali za kikanda (Igad), kwa mume wake juu ya kusafiri ndani na nje ya nchi bado yapo.
Masharti yalilenga kusitisha mapigano na kumwezesha Bw. Machar kufanya mazungumzo ya mkataba wa amani. Pia walimuwekea masharti juu ya kuongea hadharani kwa vyombo vya habari.
Mjumbe maalumu wa Igad kwa ajili ya Sudan Kusini Ismail Wais amesema kuwa masharti hayo yalipitwa na wakati wakati Bwana Machar alipochukua mamlaka mapya katika serikali ya umoja Jumamosi.
Lakini Bi Teny amesema kuwa kundi la Bwana Machar halijapokea mawasiliano yoyote kuhusiana na hilo. Amesema wanahofia huenda asiweze kutekeleza kazi zake.
Wachambuzi wanasema mkakataba baina ya Riek Machar na rais Salva Kiir si hakikisho la amani ya kudumu Sudan Kusini
Kwa mujibu wa Bi Teny, mume wake hawezi kusafiri kwa uhuru ndani ya Sudan kukutana na wafuasi wake.
Hatahivyo, msemaji wa rais Salva Kiir amekanusha madai hayo, na kuongeza kuwa Bw. Machar anapaswa kufanya mikutano ya umma na rais ili kuonyesha umoja.
Awali rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na kiongozi huyo wa zamani wa waasi Riek Machar walikubaliana kuunda serikali ya mpito ya Umoja ya Taifa, kabla ya tarehe 22 Februari.
Inaaminiwa kuwa hatua ya Machar kujiunga na serikali ya Muungano na rais Kiir itasaidia kurejesha amani ya kudumu nchini Sudan Kusini, lakini mikataba mingi ya amani imekua ikivunjwa mara kwa mara.
Baadhi ya masuala bado hayajatatuliwa, mkiwemo kugawana madaraka na suala la kuwajumuisha wapiganaji wa waasi.
Mkataba ulitangazwa saa kadhaa baada ya Umoja kuwashutumua kwa kuwa chanzo cha njaa kwa raia kwa makusudi wakati wa vita vya awenyewe kwa ajili ya kupigania madaraka.
Umoja wa Mataifa ulitoa ripoti inayozishutumu pande zote kwa kuchochea vita.
Riek Machar amekuwa hasimu wa rais Salva Kiir kwa miaka
Hakuna hakikisho.
Mikataba ya awali ilikubalika na kuvunjwa muda mfupi baadae.
Kumekua na mikataba zaidi ya 10 na makubaliano ya usitishaji wa mapigano yaliyofikiwa na viongozi waliokosana mwaka 2013 na kutokuwa na kutokuwa kwao na uwezo wa kuimarisha mkataba wowote, mkiwemo juu ya mgawanyo wa madaraka.
Peter Adwok Nyaba, mwanahakati na waziri wa zamani nchini Sudan, anasema mkataba haumalizi kikamilifu masuala yanayoibua mzozo ukabila, kupoigania mamlaka na taasisi dhaifu za utawala, ambayo anasema bado yapo licha ya mkataba.
“Huu ni mzunguko usioisha: umaskini-mzozo-amani-ukosefu wa maendeleo-halafu mzozo,” anasema.