Takriban asilimia 80 ya mapato ya Zanzibar ya kila mwaka yanatoka katika Utalii
Kisiwa cha Zanzibar hakuna mgonjwa yeyote wa virusi vya Corona licha ya kwamba uchumi wake uko hatarini kuathirika kutokana na watalii kuwa na hofu ya kusafiri kutokana na janga hilo, na wengine kutokufika visiwani Zanzibar baada ya serikali kuahirisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Itali.
Inakadiriwa kuwa takribani asilimia 80 ya mapato ya kigeni ya Zanzibar kila mwaka hutoka katika sekta ya utalii.
Lakini kutokana na janga hili la virusi vya Corona, serikali inajipanga kuimarisha uwekezaji katika sekta nyingine , kama vile uvuvi, kilimo ili kukwamua pigo hilo la kiuchumi.
Mandhari ya Zanzibar na utamaduni wake ulio na thamani huvutia takriban watalii 500,0000 katika kisiwa hicho kila mwaka.
Lakini hata hivyo kumekuwa na mabadiliko katika siku za hivi karibuni ambayo wapo walio na wasiwasi kwamba inawezekana yakawa yamesababishwa na hofu ya virusi vya Corona
Maeneo ambayo watalii hufurika yamenyamaza katika siku chache zilizopita huku hoteli kadhaa Kisiwani Zanzibar tayari zikipokea maombi ya kufuta safari, hususan kutoka kwa watalii wanaozuri kupitia makundi, Meneja wa hoteli ya Tembo Abdulaziz Yusuf amesema.
“Itatuathiri sana kwasababu tunategemea sana utalii. Soko la utalii ni soko kubwa lakini kwa jumla utalii ndio mti wa mgogo wa uchumi wa Zanzibar, hivyobasi tutapoteza mengi.”
Huku idadi ya vifo vya watu walioambukizwa ugonjwa huo ikiendelea kupanda , wamiliki wa biashara wamekuwa wakiwaonya wafanyakazi wao kutosafiri huku watalii wengi wakiamua kusalia majumbani mwao.
Yusuf Njama ni mfanyabiashara wa uongozaji watalii kisiwani Zanzibar. Anasema kwamba virusi vya korona vinaathiri pakubwa idadi ya watalii wanaozuri eneo hilo.
Asilimia 60 ya ufadhili wa kifedha wa bajeti ya Zanzibar unatoka katika sekta ya utalii.
”Lazima tuimarishe mfumo wa kilimo sasa kwa kutumia mvua tulionayo, lazima tuimarishe sekta ya uvuvi ili tusitegemee Utalii kama ilivyokuwa awali kutokana na hatari kama hii ambayo inaweza kutokea wakati wowote” , alisema waziri wa afya Hamad Rashid.
Wizara hiyo imeweka mikakati ya kusaidia kuzuia mlipuko wa ugonjwa wa viurusi vya corona , aliongezea bwana Rashid.
”Tuna vituo 192 vya afya na wafanyakazi waliopewa mafunzo ya kutafuta dalili. Tunafanya vipimo na kuzungumza na wafanyabiashara wanaosafiri kuelekea China. Ni eneo dogo, hivyobasi ni rahisi kulidhibiti”.