HABARI

Waziri Mkuu “Wote waliozuiwa sababu ya Corona wasome online”

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema wanafunzi wanaosoma katika Vyuo Vikuu mbalimbali nchini China waliozuiwa kutokana na mlipuko wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona wote wanaendelea na masomo yao kwa njia ya mtandao.
Waziri Mkuu ameyasema hayo katika mahafali ya 38 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (CKHT), katika uwanja wa Ilulu mjini Lindi ambapo amesema baada ya virusi vya corona kuikumba China vyuo vilifungwa na sasa vimefunguliwa na wanafunzi wanasoma kwa njia ya mtandao.
Waziri Mkuu amewaeleza wahitimu wa CKHT kuwa vyeti walivyotunukiwa ni tuzo halali kwa juhudi na jitihada walizoonesha katika masomo yao, hivyo wanaporejea kwenye jamii wahakikishe wanaipatia tuzo ya utendaji bora na ufanisi itakayoakisi viwango vilivyoainishwa kwenye vyeti vyao.
Waziri Mkuu amesema amewataka watambue kwamba Serikali inakiangalia kwa jicho la karibu sana Chuo Kikuu Huria kwa kuwa kimekaa kimkakati zaidi kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa na kwamba licha ya changamoto mbalimbali zilizopo, Serikali imeweza kukianzisha na kukiona kikiendelea kutanuka hadi nje ya mipaka ya nchi yetu.
Aidha amesema Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliona mbali wakati akianzisha mchakato wa kuanzisha Chuo Kikuu hicho kwa kusema angependa kuona taasisi inawawezesha watu wazima wengi waweze kuendelea na elimu ya juu pasipo kuacha kazi zao.
Katika mahafali hayo ambayo yamehudhuriwa na Waziri Mkuu Mstaafu na Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania Mizengo Peter Pinda, jumla ya wahitimu 698 wametunikiwa vyeti wakiwemo 20 wa Shahada za Uzamivu (PhD) na wengine 185 Shahada na Stashahada za Uzamili, wengine 344 walitunukiwa Shahada ya Kwanza, 166 walitunikiwa Stashahada na Astashahada mbalimbali.

About the author

kidevu

Leave a Comment