Mechi ya Manchester City dhidi ya washika bunduki wa jiji la London Arsenal imeghairishwa kufuatia hofu ya ugonjwa wa Virusi vya Corona.
Hofu imeongezeka hadi kupelekea baadahi ya vijana wa ‘the Gunners’ kujitenga baada ya mmiliki wa klabu ya Olympiakos Evangelos Marinakis kupatikana na virusi hivyo.
Taarifa kutoka ndani ya klabu ya Arsenal inaeleza kuwa baadhi ya wachezaji wake walikutana na Marinkis mwenye umri wa miaka 52 ambaye ni mmiliki wa Olympiakos Evangelos wakati wa mchezo wa kombe la Europa wiki mbili zilizopita.
Marinakis ambaye pia anaimiliki klabu ya ligi ya daraja la kwanza nchini England, Nottingham Forest alisema siku ya Jumanne kwamba amepatikana na virusi vya corona.
”Ushauri wa kimatibabu tuliopatiwa ni kwamba tayari wachezaji hao wapo katika hatari ya kupatikana na virusi hivyo, hivyo basi tumewataka kujitenga kwa muda wa siku 14 kutoka siku waliogusana na Marinakis.
Ni kutokana na hilo kwamba wachezaji hao hawatashiriki mechi iliopangwa kuchezwa dhidi ya Man City mchezo wa Premier League.
Wafanyakazi wanne wa Arsenal ambao walikuwa wameketi karibu na Marinakis wakati wa mechi hiyo pia watasalia nyumbani hadi siku 14 zitakapokamilika.