MIONGONI mwa vilio vya wanandoa wengi jijini Dar, mbali na hali ngumu ya kimaisha inayosababishwa na vyuma kukaza, matatizo ya kiafya na majanga mengine mengi, ni suala zima la uaminifu kwenye uhusiano wa kimapenzi na magonjwa ambukizi kwa njia ya ngono.
Uchunguzi uliofanywa na Gazeti la Ijumaa ulibaini kwamba, masuala ya kusalitiana yanazidi kushamiri siku hadi siku.
Imebainika kwamba, wengi waliopo kwenye uhusiano wa kimapenzi, wanalia kutokana na mateso ya usaliti.
Uchunguzi huo ulibaini kwamba, kati ya watu mia mbili, wanaoishi maeneo ya Sinza, Mwananyamala, Buguruni, Temeke, Mbagala na Kimara waliofikiwa kwenye utafiti huu, asilimia 75 (watu 151), waliweka wazi kuwahi kusalitiwa.
Ni asilimia 25 (watu 49), pekee walidai kulisikia suala la usaliti kutoka kwa jirani zao.
Pamoja na sababu nyingi ambazo Ijumaa limeelezwa kwenye utafiti huu, lakini saluni ambazo zinatoa huduma za masaji zinatajwa kuwa ni chanzo kikubwa cha usaliti na magonjwa ambukizi.
Katika maeneo hayo yaliyofikiwa, imebainika pia kuwa kati ya mitaa mitatu mpaka minne, kuna saluni moja inayotoa huduma hizo.
UTAZITAMBUAJE SALUNI ZA MASAJI NA HUDUMA ZITOLEWAZO HUMO?
Ijumaa lilikwenda mbele zaidi na kuchimba saluni hizo zinazotoa huduma za masaji. Lilibaini kwamba, zipo saluni za aina nyingi zinazotoa huduma hizo.
Zipo ambazo huandikwa jina fulani alafu mbele yake zinatambulishwa kwa maneno ‘MASSAGE’. Hizi unakuta ni katika nyumba fulani ambazo tofauti na kibao cha utambulisho unaweza kufikiri ni makazi ya mtu.
Mfano; utakuta kibao kimeandikwa Q Massage ambapo ukiingia katika nyumba hizo utapokelewa na akina dada warembo, wanaovutia ambao watakukaribisha na kukueleza aina za huduma za masaji wanazotoa.
Aina hizo ni pamoja na masaji ya kawaida. Hapa mteja anakuwa amevaa nguo zake, lakini analala kitandani, mezani au kwenye kibaraza maalum cha kufanyia masaji na anapewa huduma.
BODY TO BODY
Aina nyingine ya masaji ya mwili kwa mwili (body to body.) Katika aina hii ya masaji mteja anavua nguo zake zote na anayemhudumia anakuwa hana nguo au pengine amevaa nguo ya ndani tu!
Lakini huduma hii pia hutolewa kwenye saluni za kawaida za kiume zilizopo mitaani.
Katika saluni hizi, nyingi, bila kuwa na mteja unaweza usifahamu kama kuna huduma ya masaji inayotolewa ndani yake.
Unakuta tofauti na huduma ya kunyoa, kuremba nywele kwa mafuta ya aina tofautitofauti, ndani ya saluni hizo, kuna kichumba maalum chenye kitanda, meza kubwa au kibaraza kilichojengewa vizuri kwa ajili ya kufanyia masaji.
NGONO HUFANYIKAJE KWENYE SALUNI HIZO?
Ijumaa lilizungumza na baadhi ya watoa huduma hizo za masaji ambazo kwa jijini Dar, hutolewa kwa watu wote, wanaume kwa wanawake;
“Mteja anapokuja unaweza kumwambia kuwa masaji ni kiasi fulani, labda ile ya mwili kwa mwili. Sasa mnapoingia huko chumbani na kuanza kufanya masaji, kwa kuwa mnakuwa wawili tu na hamna nguo, baadaye anageuka na kudai kuwa amezidiwa.
“Anakutaka mfanye mapenzi na anakuongezea pesa. Kwa hiyo wengi wetu unakuta tuna shida na kiukweli kwenye sehemu za masaji, wengine wanalipwa posho za siku tu na wengine hawalipwi kabisa, ni juhudi za kila mtu kupata pesa kwa njia yoyote unapopata mteja.
“Unakuta tunashawishika na kufanya mapenzi kwa sababu ya pesa. Mtu akikolea, anachukua mawasiliano yako na mara kwa mara anakuwa anakuja kwa ajili ya kupata huduma, wakati huu unakuta hataki masaji tena, bali ngono tu,” anasema Amina, mtoa huduma ya masaji kwenye nyumba moja iliyopo maeneo ya Sinza-Kwa Remmy.
Je, ni kwa kiasi gani huduma hii ya ngono imeshamiri kwenye saluni hizi? Ni kweli kuwa machangudoa kwa sasa wamekimbilia kwenye saluni hizi? Hayo na mengine mengi usikose toleo lijalo.